Wakati sakata la kufungiwa kwa kiungo mshambuliaji Pius Buswita likiendelea kuwa gumzo hatimaye mchezaji huyo amejitokeza na kufunguka kilichotokea.
Ikumbukwe kuwa Buswita ambaye alikuwa akiichezea Mbao FC ya Mwanza, alisajiliwa na Yanga hivi karibuni lakini Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limetangaza kumfungia kwa kile ilichosema amesaini mkataba katika timu mbili za Simba na Yanga.
Akizungumzia suala hilo huku akionekana kuwa na hisia kali, Buswita amesema kuwa kilichotokea ni kuwa alilazimishwa kusaini mkataba kwenye Klabu ya Simba licha ya kuwa tayari alikuwa ameshasaini kujiunga Yanga.
Akisimulia zaidi, Buswita alisema: “Awali nilizungumza na Simba lakini hatukuafikiana, wakaja Yanga tukaelewana na nikasaini, lakini baadaye walikuja watu wa Simba na kunishawishi nisajili kwenye timu yao.
“Niliwaeleza kuwa nimeshasaini Yanga, lakini wao hawakutana kunielewa, walinilazimisha kusaini au nirudishe fedha zao za kunisafirisha kutoka Mwanza hadi Dar wakati wa mazungumzo ya awali, pia walikuwa wakinitisha ili nifanye vile walivyotaka.
“Walienda mbali zaidi na kuanza kumtisha hata mama yangu, kwani kuna muda walifika hadi nyumbani kwetu, mama yangu akawa analia na kuniambia nifanye vile wanavyotaka wao, ndiyo maana nikasaini, lakini mimi ni mchezaji wa Yanga kwa kuwa ndiyo ambao nilizungumza nao vizuri,” alisema Buswita.
No comments:
Post a Comment