Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Khairat Omary, ameishtaki Hospitali ya Kairuki na kudai fidia ya Sh milioni 155 kwa kumsababishia matatizo katika mfuko wa uzazi yaliyofanya aondolewe kizazi.
Khairat kupitia Kampuni ya Uwakili ya Jonas amefungua kesi ya madai namba 184 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Katika madai hayo, mdai anadai alikuwa akihudhuria kliniki wakati wa ujauzito katika hospitali hiyo na Desemba 15 mwaka jana alijifungua kwa upasuaji, akaruhusiwa Desemba 17 mwaka huo na kutakiwa kurudi tena Desemba 21.
Mdai akiwa nyumbani alianza kusikia maumivu ikiwamo kutapika, ilipofika Desemba 21 alirudi hospitali akaeleza maumivu anayopata kwa daktari ambaye alielekeza afanyiwe kipimo cha Ultra Sound.
Majibu yalipotoka daktari akampatia dawa za kutuliza maumivu na kumtaka apumzike hali itaendelea kuimarika.
“Akiwa nyumbani hali iliendelea kuwa mbaya, alisikia maumivu makali ya kichwa na alianza kubadilika rangi ambapo alikimbizwa hospitali ya jirani, walipompima wakaelekeza apelekwe Regency Hospital kwa matibabu zaidi.
“Regency walimfanyia vipimo na kubaini kuna tatizo katika mfuko wa uzazi na kumuhamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako pia walimfanyia vipimo na kubaini wakati alipofanyiwa upasuaji kuna vitu vilibakia kama pamba ambavyo vimesababisha mfuko wa uzazi kuharibika,” ilisema sehemu ya hati hiyo ya madai.
Anadai ili kuokoa maisha yake alishauriwa kuondolewa kizazi, hata hivyo licha ya kuondolewa alibakia na tatizo la fístula lililosababishwa na pamba zilizoachwa wakati anajifungua.
Mdai anadai kutokana na uzembe huo wa kutokuwa makini wakati wa kumzalisha anaomba mahakama iamuru alipwe Sh milioni 20 gharama za matibabu, Sh milioni 25 fidia kwa kukosa kipato wakati anaumwa, Sh milioni 80 gharama za adhabu na Sh milioni 30 fidia.
Wadaiwa wanatakiwa kupeleka utete wao mahakamani na kesi hiyo itatajwa Agost 31, mwaka huu
No comments:
Post a Comment