Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini Kenya imetangaza kwamba uchaguzi mpya wa urais nchini humo utafanyika tarehe 17 Oktoba.
Mwenyekiti
wa tume hiyo Wafula Chebukati amesema uchaguzi huo utashirikisha
wagombea wawili pekee wa urais, Rais Uhuru Kenyatta na waziri mkuu wa
zamani Raila Odinga."Hakutakuwa na uteuzi mpya wa wagombea wa urais katika uchaguzi huo upya. Waliopinga matokeo ya uchaguzi kortini, Bw Raila Odinga na mgombea mwenza wake Stephen Kalonzo Musyoka na mshtakiwa wa tatu Rais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Samoei Ruto, watakuwa ndio wagombea pekee," taarifa ya bw Chebukati imesema.
Katika kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Mahakama ya Juu iliiwekea lawama Tume ya Uchaguzi.
- Mambo kumi yasiyofaa kukupita kuhusu uchaguzi mkuu Kenya 2017
- Upinzani Kenya wadai Odinga ndiye mshindi wa urais
Bw Chebukati amesema tume hiyo inafanyia utathmini mifumo na taratibu zake kwa ajili ya uchaguzi huo mpya.
Mwenyekiti huyo hata hivyo ametoa wito kwa Mahakama ya Juu kutoa hukumu ya kina kuhuhusu kesi iliyowasilishwa na Bw Odinga kupinga ushindi wa kenyatta ili kuiwezesha "tume kutambua maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa katika usimamizi wa uchaguzi mpya".
Majaji wa mahakama ya juu waliahidi kutoa hukumu kamili kabla ya tarehe 22 mwezi huu.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na IEBC kuhusu uchaguzi uliofanyika tarehe 8 Agosti, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.
Upinzani ulipinga matokeo hayo ukisema mitambo ya tume hiyo ya uchaguzi iliingiliwa kumfaa Bw Kenyatta
No comments:
Post a Comment