Niyonzima: Acheni Utani, Yanga Hii Ni Hatari
KIUNGO wa Simba, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, amesema kuwa, endapo muunganiko wa Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Papy Tshishimbi na Thabani Kamusoko utatimia, basi kuna uwezekano mkubwa wa kuipa ubingwa timu yao ya Yanga.Niyonzima ambaye Jumamosi iliyopita aliichezea Simba mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara tangu ajiunge nayo akitokea Yanga, amesema pamoja na timu yake hiyo kupata ushindi wa mabao 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, wanaweza kukutana na kikwazo cha kuwa mabingwa kutoka kwa Yanga kwa kuwa wanaonekana wapo vizuri sana tofauti na watu wanavyodhani.
Akizungumza na Championi Jumatano, Niyonzima amesema kuwa watu wengi wameanza kuonyesha wazi kuibeza Yanga kutokana na sare iliyoipata Jumapili dhidi ya Lipuli ya Iringa, jambo ambalo kwake haoni ni sawa kwani anaamini Yanga bado ina kikosi kizuri.
“Kwa sasa nipo Simba, timu yangu ambayo ina kila kitu na inafanya vizuri, ila hakuna ubishi kuwa kama wachezaji wenzangu wataanza kufanya utani kwa kuibeza Yanga kutokana na matokeo waliyoyapata mwishoni mwa wiki iliyopita, basi watakuwa wanajidanganya kwani muunganiko wa Tshishimbi na Kamusoko utakapokaa vizuri, nina imani watatisha sana ligi hii.
“Mbali na hao, pia watu wanatakiwa kukubaliana na mimi kuwa Ngoma ni mchezaji mzuri na msumbufu sana uwanjani, hivyo atakapopona Chirwa na Tambwe, hakika watatusumbua sana tofauti na wengi wanavyodhani kwamba kutoka sare kwa Yanga kutaifanya ishindwe kutetea taji lake.
“Kikubwa mimi ninachoweza kukisema hapa klabu yangu ya Simba inatakiwa tulitambue hili na tuendelee kukaza kila mchezo wetu ili tuweze kuibuka na pointi tatu muhimu kwani njia pekee ya kufikia mafanikio tuliyojipangia ni kuendeleza kuvuna ushindi katika kila mechi iliyo mbele yetu na tuachane na kuwabeza Yanga ambao mimi nafahamu uzuri wao ulipo.
“Kwa sasa utaona Yanga inateseka kupata mabao kutokana na nafasi ambayo Ngoma amekuwa akichezeshwa pamoja na Raphael Daudi, ila atakapokuja kuanza Chirwa ambaye ni msumbufu kama yeye hakika timu yao itabadilika,” alisema nahodha huyo wa Rwanda.
Na Musa Mateja, Dar es Salaam
Source : Global Publishers
No comments:
Post a Comment